Mwongozo wa kutumia Kamusi TUKI ya Kiswahili-Kiingereza

Utangulizi

Kamusi ya Kiswahili–Kiingereza imekusudiwa kuwasaidia watu wanaojifunza Kiingereza au Kiswahili. Ili kukidhi haja hiyo, msamiati unaotumika katika mawasiliano ya kawaida miongoni mwa wanajamii umeteuliwa na kuingizwa katika kamusi. Msamiati unaoingizwa katika kamusi ili na kufasiliwa huitwa kidahizo ( wingi wake ni vidahizo).Vidahizo hufafanuliwa kwa kupatiwa taarifa mbalimbali ambazo mwanafunzi wa lugha anazihitaji ili kumwezesha kupata umilisi wa kuiongea na kuiandika lugha. Baadhi ya taarifa hizi zimeingizwa kwa alama au misimbo ambayo sio rahisi kwa mtumiaji asiyekuwa na maarifa ya kutumia kamusi kuweza kuisimbua na kuelewa taarifa iliyofumbwa. Mwongozo huu unaonyesha namna sehemu kuu za kitomeo na taarifa mbalimbali zinazohusu lugha zilivyoingizwa katika kamusi hii. Lengo la kuonyesha taarifa hizi ni kumwezesha mtumiaji kamusi ajue taarifa zilizomo na jinsi zilivyoingizwa ili afahamu namna atakavyoweza kuzipata (kuzisimbua). Maelezo yafuatayo yanamwelekeza mtumiaji kamusi namna ya kuitumia kamusi hii.

Kidahizo

Kidahizo ni neno linaloingizwa katika kamusi ili lifafanuliwe kwa kupatiwa maelezo yanayohusu taarifa za kisarufi, maana, matumizi, etimolojia, semi mbalimbali za lugha n.k. Vidahizo vya kamusi hii ni maneno ya kawaida ya Kiswahili yanayotumika katika nyanja mbalimbali za mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji wa Kiswahili. Msamiati huu umetokana na Kiswahili sanifu na umekusanywa kutoka matini za msingi za Kiswahili sanifu, kama vile kamusi za Kiswahili zilizopo: TUKI (1981) Kamusi ya Kiswahili Sanifu, TUKI (2001) Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo jipya), Johnson (1939) Kamusi ya Kiswahili–Kiingereza na Feeley (1990) Kamusi ya Kiswahili–Kiingereza.Maneno mengine yametokana na orodha ya msamiati wa fani mbalimbali ulioundwa au kusanifiwa na BAKITA, na kutumiwa kufundishia katika shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu. Msamiati ulioingizwa kama vidahizo ulikusanywa pia kutoka magazeti ya Kiswahili na vitabu vya riwaya, tamthiliya na mashairi ya Kiswahili vilivyochapishwa Kenya na Tanzania.. Kwa hivyo msamiati uliomo humu unawakilisha Kiswahili kinachoongewa Afrika ya Mashariki. Kamusi ina vidahizo vya aina mbili: 1) kidahizo kikuu, na 2) kidahizo mfuto.

Kidahizo kikuu

Neno linaloingizwa kama kidahizo kikuu, kwa kawaida huwa ni umbo la msingi la neno. Kinyambuo huingizwa tu iwapo imedhihirika kuwa kina matumizi mapana au maana yake inatofautiana na maana ya umbo la msingi kiasi kwamba mwanalugha atashindwa kudadisi maana yake kutokana na maana ya umbo mama na kulazimika kulitafuta katika kamusi.Vidahizo vingi katika kamusi hii ni neno mojamoja isipokuwa vichache tu ambavyo ni maneno ambatani yenye kuwakilisha dhana moja:

mama mkwe
mlango wa fahamu
pimajoto

Kidahizo mfuto

Kidahizo mfuto ni kinyambuo kisichotumika sana au neno ambatani ambalo limeingizwa ndani ya maelezo ya kidahizo kikuu (ambacho ni umbo la msingi) na kutolewa maelezo ya maana na ya kisarufi. Iwapo halitumiki sana au halijapata kutumika lakini huenda likatumika siku moja hupatiwa maelezo ya kisarufi pekee. Kinyambuo cha kitenzi ambacho kina kategoria tofauti huingizwa kama kidahizo mfuto ndani ya umbo la msingi bila maelezo ya maana na kisha huingizwa tena kama kidahizo kikuu katika herufi ya alfabeti inayohusika.

agu.a kt [ele]…….(tde) agulia, (tdk) agulika, (tdn) aguana. mwaguzi nm. uaguzi nm.
mama nm [a-/wa-] mother: ~ mkubwa mother’s elder sister; ~ mdogo mother’s younger sister; ~ wa kambo step mother.

Vinyambuo vya kitenzi agua na nomino ambatani zinazotokana na nomino mama (kama vitomeo ‘agua’ na ‘mama’ hapo juu vinavyoonyesha) zimeingizwa kama vidahizo mfuto.Vinyambuo huandikwa kwa chapa iliyokoza na maneno ambatani huandikwa kwa chapa ya italiki.

Mpango wa vidahizo katika kamusi

Vidahizo vimepangwa kwa kufuata utaratibu wa kialfabeti. Kwa kila ukurasa neno la kwanza na la mwisho katika ukurasa limechapwa katika sehemu ya juu ya ukurasa ili kumwongoza msomaji atambue nafasi ya neno analolitafuta, iwapo lipo katika ukurasa anaousoma, au lipo nyuma au mbele ya ukurasa unaohusika. Maneno ya kumwongoza msomaji humwezesha kuipitia kamusi upesi na kugundua neno analolitaka kuliko kusoma kila ukurasa na kila kidahizo ili kupata neno analolitafuta.

Tahajia kibadala ya kidahizo

Kidahizo chenye kibadala huingizwa pamoja na kibadala chake. Kwanza kidahizo huandikwa na kisha kibadala hufuata kikitanguliwa na neno ‘pia’ au ‘tazama’ lenye kudokeza kuwa neno linalofuata ni kibadala, halafu hufuatia kategoria ya kisarufi:

hemer.a pia heme.a kt
hususa pia hususan kl
maandishi pia maandiko nm

Kurejeleana vidahizo

Kidahizo chenye kibadala ambacho kimeingizwa katika kamusi kimepewa neno la kurejeleana ambalo humwelekeza msomaji kwenye kibadala chake. Neno la kurejeleana lililotumika katika kamusi hii ni pia na tazama ambalo limeandikwa kwa kifupi taz.

Homonimu

Homonimu ni maneno ambayo maumbo yake yanafanana lakini maana, etimolojia na kategoria zao za kisarufi ni tofauti. Maneno ambayo ni homonimu yanachukuliwa kuwa ni maneno tofauti na kila moja huingizwa kama kidahizo tofauti katika kamusi. Ili kuvitofautisha vidahizo ambavyo ni homonimu, kila kimoja kimepewa namba ya peke yake:

Kitomeo

Kitomeo ni aya ndogo katika kamusi ambayo ina kidahizo na taarifa zote zinazohitajika kukifafanua. Kitomeo kinaanza na kidahizo ambacho huandikwa kwa chapa iliyokoza. Kila kidahizo kina aya yake. Taarifa zinazoingizwa katika kila aya hutegemea kategoria ya kidahizo. Ijapokuwa kila kidahizo hupatiwa taarifa za msingi zinazofanana, baadhi huwa na taarifa nyingi zaidi. Hii ndio maana vidahizo vingine vina aya ndefu na vingine aya zake ni fupi. Taarifa iliyo katika aya ya kidahizo ni kielelezo cha taarifa zinazoingizwa katika kamusi:

me.a kt [sie]1 sprout, germinate, sprint: Mbegu haziku~ the seeds did not germinate. 2 grow, develop a new growth on the human body: Kucha zime~ mno the nails have overgrown. (nh) ~ meno be arrogant. (tde) melea; (tdk) meka; (tds) mesha.

Taarifa muhimu zilizoingizwa katika kamusi hii ni: taarifa za kisarufi, visawe vya Kiingereza kwa maneno ya Kiswahili (maana), mifano ya matumizi kwa lugha zote mbili, nahau, misemo, etimolojia, vinyambuo, mzizi wa kitenzi n.k.

Etimolojia ya kidahizo

Vidahizo vyenye asili ya kigeni huashiriwa kwa nyota, na kisha kifupisho cha lugha chasili huingizwa mwishoni mwa kitomeo. Lugha zilizochangia msamiati wake katika Kiswahili ni pamoja na Kiarabu ambayo kifupisho chake ni (Kar), Kiajemi (Kaj), Kiingereza (Kng), Kijerumani (Kje), Kireno (Kre). Kifaransa (Kfa), Kihindi (Khi) n.k.

mez.a2 kt [ele] swallow (up). 2 engulf. (tde) mezea; (tdk) mezeka; (tdn) mezana;(tds) mezesha; (tdw) mezwa.

Taarifa za Kisarufi

Kila kidahizo kinaainishwa kategoria ya kisarufi inayokihusu na kuashiriwa. Iwapo kidahizo kina uamilifu kwa kategoria zaidi ya moja, huashiriwa kategoria zote zinazokihusu. Aina mbili za kategoria zimeingizwa katika kamusi hii. (1) Kategoria kuu: nomino (nm), kitenzi (kt), kivumishi (kv), kiwakilishi (kw), kielezi (kl), kihusishi (kh), kiingizi (ki) na kiunganishi (ku) na (2) Kategoria ndogo, ambayo hupambanua kwa undani zaidi tofauti ndogondogo za kategoria kuu. Kila kidahizo kimeainishwa kategoria yake kuu isipokuwa vidahizo ambavyo ni nomino au vitenzi ambavyo vimeainishwa kategoria ndogo pia. Nomino zimeonyeshwa pia umoja na wingi pamoja na vipatanishi vitenzi vya nomino inapojaza nafasi ya kiima katika sentensi. Vitenzi hubainishwa pia iwapo ni elekezi [ele] au sielekezi [sie].

Kidahizo cha Nomino

Kidahizo cha nomino hupatiwa alama ya kuashiria kategoria ya kisarufi nm na kiambishi chenye kuwakilisha umbo la wingi la nomino ambacho kwa kawaida huwa ni silabi ya kwanza ya umbo la wingi. Nomino ambayo haina umbo la umoja wala wingi, au yenye kutumika katika umbo la umoja tu au umbo la wingi tu haikupatiwa alama yoyote:

mpembuzi nm wa-
udongo nm
mkono nm mi-
maji nm

Kwa nomino yenye umoja na wingi ambayo umbo la wingi lina mabadiliko kidogo, umbo zima la wingi huingizwa baada ya umbo la umoja:

wadhifa nm nyadhifa
ua nm nyua
ukuta nm kuta

Kidahizo cha nomino hupatiwa pia vipatanishi vitenzi vya nomino (kwa umbo la umoja na wingi) vyenye kuleta upatanisho wa kisarufi baina ya nomino na kitenzi viwapo katika sentensi ya Kiswahili. Kwa mfano: Mpambe amewasili, Wapambe wamewasili wote. Kikombe kimevunjika, Vikombe vimevunjika. Embe limeoza, Maembe yameoza. Nyumba imejengwa, Nyumba zimejengwa

kikombe nm [ki-/vi-]
embe nm ma- [li-/ya-]
nyumba nm [i-/zi-]

Kidahizo ambacho kina uamilifu kwa nomino na kategoria nyingine, uamilifu wa nomino huonyeshwa kwanza kisha zikafuata nyingine:

ajabu nm ma- [i-/ya-] wonder…….: Ma~ ya dunia
the wonders of the world. kv extraordinary,
stupendous, wonderful. Mtu wa ~ a wonderful
person. kl strangely, extraordinarily; too much:
Jua ni kali ~ the sun is just too hot.

Kidahizo cha kitenzi

Kitenzi cha Kiswahili kama zilivyo lugha zote za Kibantu kina tabia ya kunyumbuka na kuzalisha maumbo mengine mengi yenye kushiriki mzizi mmoja.

Mzizi wa Kitenzi

Mzizi wa kitenzi ni sehemu ya neno ambayo hubakia baada ya kumegua viambishi vyote vilivyoambatishwa. Katika kamusi hii mzizi wa kila kitenzi umetengwa na viambishi kwa nukta (kitone ) ili kumwonyesha mtumiaji kamusi mzizi wa kitenzi ambao ukiambatishwa viambishi tofauti huweza kuunda maneno mengine tofauti. Kwa hivyo kitone ndio mpaka baina ya mzizi na viambishi:

teg.a > teg.ea, teg.eka, teg.ana, teg.esha, teg.wa.
tazam.a > tazam.ia, tazam.ika, tazam.ana, tazam.isha, tazam.wa

Kitenzi kilichoingizwa kama kidahizo kimepatiwa alama ya kategoria yake ya kisarufi ambayo ni kt, taarifa ya uelekezi na vinyambuo vya kitenzi, nomino au vivumishi vinavyoweza kuzalishwa kutokana na kitenzi kinachohusika. Itafaa kusisitiza hapa kuwa vitenzi havina uwezo wa kuzalisha idadi sawa ya vinyambuo.

Vitenzi vyenye asili ya Kibantu huishia na herufi –a kama mifano ya vitenzi hapo juu inavyoonyesha. Vitenzi vinavyoishia na irabu nyingine kama vile -e, -i na -u vimeingizwa katika Kiswahili kama vilivyo kutoka lugha za kigeni ambazo zina utaratibu tofauti wa kunyumbua maneno na kuunda maneno mapya. Ijapokuwa irabu katika vitenzi hivi ni sehemu ya mzizi katika lugha chasili, vitenzi hivi vimechukua tabia ya unyumbuaji vitenzi ya lugha za Kibantu ya kutenga irabu ya mwisho na kuzalisha vinyambuo kama maneno mengine ya Kiswahili. Kwa hali hiyo irabu ya mwisho ya vitenzi vya mkopo katika kamusi hii nayo imetengwa pia.

stareh.e >stareh.ea, stareh.eka, stareh.esha
jib.u > jib.ia, jib.ika, jib.isha

Vitenzi vya mkopo ambavyo vimeghairi kufuata mfumo huu ni vichache sana. Vitenzi hivi havibagui irabu ya mwisho na vinaponyambuliwa, huambatishwa tu viambishi tamati.

sahau > sahau.lia, sahau.lika, sahau.lisha.

Kinyambuo

Kinyambuo ni umbo la neno ambalo huundwa kwa kuambatisha viambishi kwenye mzizi. Katika Kiswahili mzizi wa kitenzi ndio wenye kunyambuliwa na kuzalisha vitenzi vingine na nomino kuliko kategoria nyingine za maneno. Katika kamusi hii vinyambuo vimeonyeshwa kwa kila kitenzi na kuorodheshwa mwishoni mwa kitomeo pamoja na kategoria zao za kisarufi:

agu.a kt [ele] ... (tde) agulia; (tdek) agulika, (tdew) aguliwa; (tdn) aguana. mwaguzi nm. uaguzi nm.

Mzizi wa kitenzi cha Kiswahili huweza kunyumbuliwa na kuunda vinyambuo vitenzi kadha. Hapa tumeingiza vinyambuo vitenzi vya msingi vitano: kinyambuo tendea (tde), kinyambuo tendeka (tdk), kinyambuo tendana (tdn), kinyambuo tendesha (tds) na kinyambuo tendwa (tdw). Tabia ya vitenzi vya Kiswahili ni kuwa kinyambuo kitenzi kinaweza pia nacho kikanyumbuliwa zaidi na kuzalisha vinyambuo vingine. Hii ndio sababu katika kitomeo cha kitenzi agua hapo juu, (tde) ni agulia, ambayo imefuatwa na (tdek) agulika na (tdew) aguliwa. Hii ina maana kwamba kinyambuo agulia kimezalisha vinyambuo agulika na aguliwa.

Unyambuaji wa vitenzi vya Kiswahili

Mzizi wa kitenzi unaponyambuliwa na kuzalisha kinyambuo, shina la kinyambuo hiki nalo hunyambuliwa zaidi na kuunda kinyambuo ambacho kikinyambuliwa tena nacho huzaa kinyambuo kingine. Vitenzi vyenye uwezo wa kuzalisha vinyambuo mara tatu kutoka kwenye mzizi mmoja ni vichache sana:

pig.a > (tde) pig.i.a, (tdk) pig.ik.a, (tdn) pig.an.a, (tds) pig.ish.a, (tdw) pigw.a.
pig.an.
a > pig.an.i.a, pig.an.ik.a, pig.an.ish.a, pig.an.w.a.
pig.an.ish..a > pig.an.ish.i.a, pigan.ish.w.a

Kutokana na mzizi wa pig.a tumeweza kunyambua na kuunda vinyambuo kwa hatua tatu:

Pig.a > pig.an.a > pig.an.ish.a > pig.an-ish.w.a

Kidahizo cha Kivumishi, Kielezi, Kiwakilishi, Kiingizi, Kihusishi, na Kiunganishi.

Vidahizo vya aina hizi za maneno hubainishwa kwa kategoria kuu ya kisarufi inayohusika yaani kv kwa kivumishi, kl (kielezi), kh (kihusishi), ku (kiunganishi), kw (kiwakilishi).

kabisa kl
kwa kh

Visawe vya Kiingereza

Maelezo ya maana kwa vidahizo vya kamusi ya lugha mbili ni visawe katika lugha inayolengwa. Juhudi zimefanywa kupata kisawe ambacho ni neno moja na pindi iliposhindikana, kiliteuliwa kirai chenye kubeba maana sawa na kisawe. Mara chache fasili ilitolewa badala ya kisawe. Hii ilitokea tu iwapo Kiingereza hakina neno lenye maana sawa na neno la Kiswahili. Wakati mwingine fasili ilitolewa pamoja na kisawe ili kufafanua kisawe kilichotolewa.

pacha nm ma- [a-/wa-] twin
pakanga nm [i-/zi-] labour pains
pemba kt [ele] 1 deceive, outwit, flatter with fine words.

Visawe vya kidahizo chenye maana moja inayoelezwa kwa visawe viwili au zaidi vimetengwa kwa alama ya mkato.

manati nm [ya-] catapault, slingshot

Iwapo visawe vina maana inayoachana kidogo, hutengwa kwa nukta mkato. Maana tofauti za kidahizo zimebaguliwa kwa tarakimu.

manukato nm [ya-] perfume; anything with a sweet scent.
malipo nm [ya-] 1 payments. 2 recompense, revenge.

Mifano ya matumizi

Tungo za mifano zimetolewa kwa baadhi ya vidahizo ili kuonyesha jinsi neno linavyotumika katika muktadha halisi wa matumizi ya lugha. Mifano ya matumizi imeingizwa baada ya maelezo ya maana ambayo yamefuatiwa na nukta mbili (:) na kuandikwa kwa italiki.Katika mfano wa matumizi nafasi ya kidahizo huonyeshwa kwa alama ya wimbi (~):

ach.a kt [ele] 1 quit/stop doing sth, recant, desist: ~ ulevi quit/stop drinking. 2 leave behind: Wasafiri wame~ mizigo yao nyuma passengers left their luggagge behind.
pa.a kt [ele] ~ moto transfer embers, convey fire by getting a live ember on a sherd.
pengine kl 1 perhaps. 2 somewhere else: Hapa hawauzi mafuta jaribu ~ they do not sell oil here, try somewhere else.

Dhima ya tungo za mifano ni pamoja na kuonyesha maneno yanayoambatana na kidahizo. Kwa mfano paa huambatana na mkaa katika maana iliyo kwenye muktadha huu na sio neno jingine kama vile hamisha. Tungo za mifano ya matumizi zimetumiwa pia ili kumwonyesha mtumiaji upatanisho wa kisarufi unavyojidhihirisha katika Kiswahili. Katika mfano wa kidahizo acha: Wasafiri wameacha mizigo yao nyuma, upatanisho wa kisarufi baina ya nomino wasafiri na kitenzi wameacha unaonekana. Halikadhalika baina ya mizigo na yao.

Tungo za mifano katika kamusi hii hutokea baada ya kisawe kama ilivyo kwa mifano acha na pengine hapo juu, lakini wakati mwingine zimeingizwa mara baada ya taarifa za kisarufi iwapo neno lenyewe halina maana isipokuwa linapokuwa katika muktadha tu kama mfano wa kitomeo unavyoonyesha. Kila tungo ya mfano ilitafsiriwa pia ili kumpatia mwanafunzi wa Kiingereza sentensi katika lugha lengwa ambayo ni tafsisri ya tungo ya Kiswahili anachokifahamu.

Nahau, Misemo na Methali

Nahau, misemo na methali ni tungo funge zenye maana ambayo haitokani na maana za maneno yaliyo katika tungo. Nahau nyingi za Kiswahili zinaundwa na kitenzi kama neno kuu:

aga dunia die
chungulia kaburi be very near death
kata choo interupt
hana kaba ya ulimi s/he can’t keep a secret

Misemo ni semi zenye mafundisho yenye busara ambazo hutolewa kwa mafumbo ambayo mjuzi wa lugha ndiye awezaye kutegua fumbo na kuelewa ujumbe uliobebwa na maneno hayo: Asiyejua maana haambiwi maana don’t argue with a fool

Mkwara hauhitaji mafuta a beautiful person needs no decoration
Usinivishe kilemba cha ukoka don’t flatter me
Uking’wafua mnofu ukumbuke na kuguguna mfupa whenever you are in happiness remember that there are unhappy times as well.

Kwa kuwa nahau na misemo ni semi zilizojikita katika utamaduni wa lugha, zimeingizwa humu ili kumfahamisha mwanafunzi wa Kiswahili vionjo vya lugha hii ambavyo humfanya mweledi wa kuizungumza aiongee kisanii. Kwa hali hyo, maelezo ya semi hizi katika Kiingereza ni tafsiri tu ya semi za Kiswahili ili kumpatia msomaji maana yake na wala sio visawe vya semi katika Kiingereza.

Methali kama zilivyo semi za lugha zimefungamana sana na utamaduni wa jamii inayoongea lugha hiyo. Kwa hali hii methali katika lugha moja huenda ikakosa kisawe katika lugha nyingine kwa sababu kile jamii moja inachokiona kuwa ni maadili mema ya kufunza, jamii nyingine huenda ikayaona sio muhimu. Katika kamusi hii methali za Kiswahili zimeingizwa na kupatiwa tafsiri yake katika Kiingereza:

Mkokoto wa jembe si bure yao hard work pays.
Asiye mkoma hujikoma mwenyewe one who has no assistance should self assist.

Matumizi ya misimbo na alama katika kamusi

Katika kamusi hii misimbo na alama mbalimbali zimetumiwa kueleza taarifa zilizoingizwa.

1) Ufafanuzi wa muktadha wa matumizi na maana ya maneno uliowekwa katika mabano.

Ufafanuzi ulio katika mabano umeingizwa katika kamusi ili kuonyesha kikomo cha matumizi ya neno, hadhi ya neno au maelezo ya ziada ya kufafanua maana. Kwa mfano:

Ufafanuzi wa kikomo cha matumizi

mabadiliko (uganga) climateric.
mamba (Marekani) alligator.

Ufafanuzi wa hadhi ya neno

mabishano (zamani) argy-bargy, controversy.
makame (zamani) headman, traditional Pemba ruler.

Ufafanuzi wa maana.

mama mkuu (katika nyumba ya watawa) abbess.
mjomba a Swahili (called so by the people of the hinterland).

2) Alama za mabano ya duara ( ) na mraba [ ] zimetumika kutenga taarifa za kileksikografia zilizoingizwa kwa misimbo katika kitomeo ili zisimkanganye msomaji.

Mabano ya duara ( ) yametumika kufunga ufafanuzi wa maana na matumizi ya neno ili kuutenga na fasili au kisawe. Mabano haya yametumika pia kufunga kifupisho cha lugha ambamo kitomeo kimekopwa na kuitenga na maelezo mengine katika kitomeo. Aidha mabano haya yametumika katika kutenga kiambishi cha wingi katika Kiingereza.

mbuji authority (in a certain field / subject)
mama mkuu (katika nyumba ya watawa) abbess
mbegu seed(s)

Mabano ya mraba [ ] yametumika kufunga taarifa za kisarufi zilizoingizwa msimbo kaitka kategoria za nomino na kitenzi. Kategoria ndogo ya kisarufi ya nomino yenye kudokeza upatanisho wa kisarufi baina ya nomino (kama kiima) na kitenzi (katika kiarifu) imetengwa na alama ya kategoria ndogo ya kisarufi yenye kudokeza wingi wa nomino.

mbadhirifu wa-[a-/wa-]
mbaruti mi- [u-/i-]
mbegu [i-/zi-]

Kategoria ndogo ya kisarufi yenye kubainisha uelekezi wa kitenzi imetengwa na alama ya kategoria kuu ya kitenzi.

chez.a kt [ele]
simam.a kt [sie]

Alama za uandishi: mkato (,), nukta (.), nukta mkato (;), nukta mbili (:), alama ya wimbi (~), alama nyota *, na alama ya mshangao (!) zimetumiwa katika kamusi hii kuashiria taarifa fulani:

a) Mkato umetumika kutenga visawe vya kitomeo ambavyo ni sinonimu;

b) Nukta imetumika kutenga mzizi wa kitenzi na irabu ya mwisho na pia kuashiria mwisho wa maana ya kidahizo ambacho ni polisemi, au mwisho wa kitomeo;

c) Nukta mkato hutenga visawe ambavyo maana yake imeachana kwa kiasi fulani japokuwa tofauti zao hazijawa kubwa kustahili hata kulifanya neno kuwa polisemi. Alama hii hutenga tungo za mifano zinazofuatana katika kitomeo, nahau, misemo na vinyambuo vya kitenzi;

d) Nukta mbili hutenga visawe na mfano wa matumizi katika kitomeo;

e) Alama ya wimbi katika tungo huonyesha nafasi itakayojazwa na kidahizo;

f) Nyota hudokeza kuwa neno linaloashiriwa linatokana na lugha ya kigeni ambayo kifupisho chake kimeingizwa mwishoni mwa kitomeo.

aali* kv (vitu) superior, great; exalted: Haya ni mambo ~ these are (exalted) great things. (Kar)

g) Alama ya mshangao ni ishara kuwa kidahizo ni kategoria ya kiingizi.

Matumizi ya tarakimu

Tarakimu zimetumika kwa namna mbili.

Tarakimu ndogo inayofuata kidahizo na kuinuliwa juu kidogo, huashiria idadi ya vidahizo ambavyo ni homonimu.

abir.i1 kt [ele]
abir.i2 kt [ele]
abir.i3 kt [sie]

Tarakimu zinazoingizwa ndani ya kitomeo hutenga maana tofauti za kidahizo.

abud.u kt [ele]1 worship. 2 idiolize. 3 adore, love.

Tarakimu zilizo kwenye mabano zimetumika kutenga nahau tofauti zilizo katika kitomeo kimoja.

kata kt [ele]… (nh) (1) ~ choo interrupt sb; (2) ~ hamu satisfy appetite; (3) ~ shauri conclude.

Vifupisho vilivyo katika kamusi

  • [ele] = elekezi
  • Kaj = Kiajemi
  • Kar = Kiarabu
  • Kbr = Kiibrania
  • Kch = Kichina
  • Kfa = Kifaransa
  • kh = kihusishi
  • Khi = Kihindi
  • Khs = Kihispania
  • ki = kiingizi
  • Kje = Kijerumani
  • Kla = Kilatini
  • Kng = Kiingereza
  • Kre = Kireno
  • kt = kitenzi
  • ku = kiunganishi
  • kv = kivumishi
  • kw = kiwakilishi
  • (ms) = msemo
  • (nh) = nahau
  • nm = nomino
  • [sie] = sielekezi